Jumatano , 10th Oct , 2018

Mkuu wa Usalama barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Marison Mwakyoma, amesema watu wasijadili jambo kishabiki badala yake wasikilize wataalam, kama ambavyo Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola ametoa pendekezo kuhusu bodaboda kuwa na matela.

Mkuu wa Usalama barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Marison Mwakyoma na Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola.

Akiongea leo kwenye kipindi cha East Africa Drive kinachoruka kupitia East Africa Radio kila siku za Jumatatu mpaka Ijumaa, Mwakyoma ameweka wazi kuwa waziri ana mamlaka ya kutoa pendekezo la kupunguza foleni jijini Dar es salaam ndio maana akaja na wazo la pikipiki za matela.

''Unajua watu wanajadili vitu kishabiki bila kujua IGP na Waziri wana mamlaka kisheria ya kutoa pendekezo ili kumaliza tatizo la foleni na baada ya hapo ndipo hatua zingine zinafuata kwaajili ya kuona kama wazo hilo litafanyakazi'', amesema.

Mwakyoma amebainisha kuwa kuna sheria inayoruhusu mtu kubadilisha usajili wa usafiri wake kutoka kubeba mizigo hadi watu au idadi ya watu lakini ni jinsi gani ya kukiandaa ndio inazingatiwa kwa kuwahusisha shirika la viwango TBS na msajili wa vyombo vya usafiri.

Julai 7, 2018 katika maonyesho ya kimataifa ya biashara maarufu Sabasaba, Waziri huyo wa Mambo ya Ndani alieleza mkakati wake wa kupunguza ajali za pikipiki kwa kuja na mpango wa kuzifanya pikipiki ziwe na matela ili kuzipunguza ajali za bodaboda mjini.