Alhamisi , 22nd Sep , 2022

Mkoa wa Kagera umeanza kuchukua hatua za kuimarisha uchunguzi na kuwapima afya kwa kutumia mashine wasafiri wote wanaoingia nchini kupitia katika mipaka yote, ili kudhibiti ugonjwa wa Ebola usiingie nchini, baada ya kugundulika kuwepo kwa ugonjwa huo katika wilaya ya Mubende nchini Uganda

Akizungumza na EATV mganga mkuu wa mkoa wa Kagera Dk. Issessander Kaniki amesema kuwa mbali na kuimarisha vipimo na uchunguzi katika mipaka yote, pia wanatoa elimu kwa wananchi wotewenyeviti wa vitongoji na vijiji, watendaji wa vijiji na kata na watumishi wa afya walioko mipakani juu ya namna ya kudhibiti ugonjwa huo.

Aidha Dk. Kaniki amesema kuwa wamekwishaanisha maeneo ya dharura kwenye mipaka yote, ambayo yanaweza kutumika endapo litatokea tatizo, na kwamba maeneo hayo yanaendelea kuimarishwa kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa huo.

"Ugonjwa huu uligundulika nchini Uganda katika wilaya ya Mbende, hii ni wilaya ambayo inapakana kabisa na mkoa wa Kagera, kupitia wilaya za Kyerwa, Karagwe, Missenyi na Bukoba, lakini pia katika visiwa karibia vyote vilivyoko katika wilaya ya Muleba, tumechukua tahadhari zote katika mipaka yote rasmi na isiyo rasmi" amesema Dk. Kaniki
Baadhi ya wananchi waliozungumzia ugonjwa huo wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hasa waishio mipakani, ili wasiruhusu watu kuingia kupitia njia za panya.

"Ebola ni ugonjwa tishio, ni sawa sawa na Corona, kwa hiyo tusipofanya udhibiti mapema, endapo utaingia itakuwa shida kubwa kwa wananchi hasa kwa upande wa matibabu, kwa hiyo tunaweza kupoteza wananchi na nguvu kazi ya taifa" wamesema wananchi.

Baadhi ya dalili za ugonjwa huo ni homa kali, kichefucheu na kutapika, kuharisha, kuumwa kichwa, maumivu ya misuli, mwili kuchoka, kukosa hamu ya kula na kutokwa na damu sehemu za wazi kama mdomo na pua.
Serikali ya Uganda tayari imethibitisha kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola nchini humo, baada ya mtu mmoja kupoteza maisha katika wilaya ya Mubende