Jumapili , 9th Jan , 2022

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda amewataka Watanzania kupuuzia taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa jeshi hilo kupitia Mkuu wa Majeshi limeingilia sakata la mhe. Spika.

"JWTZ linawaomba Umma wa Watanzania kutoziamini taarifa hizo na wazipuuze kwa kuwa ni taarifa za uzushi na uchochezi zinazotungwa na kusambazwa na kikundi cha watu wasioitakia mema nchi yetu kwa maslahi yao binafsi, Mkuu wa Majeshi hajatoa taarifa yoyote kuhusiana na yaliyozushwa kwenye mitandao"

"JWTZ halijihusishi kwa njia yoyote ile na masuala ya kisiasa na kamwe halitafanya hivyo" - Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano JWTZ

Aidha Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda amesema, "Daima JWTZ litamlinda na kumtii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu''.

"JWTZ linatoa onyo kwa wale wote wanaotumika kumchafua Mkuu wa Majeshi, kwa lengo la kutaka kuliingiza Jeshi kwenye siasa, kamwe Watu hao hawatafumbiwa macho na pindi watakapobainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ili liwe fundisho kwa wengine".

Pia amesisitiza kuwa "Tunawaomba watanzania wote kuungana kwa kuendelea kupuuza na kukemea vikali taarifa hizo ambazo hazilitakii mema Taifa letu, nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania wote kwamba JWTZ lipo imara, linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa mujibu wa Katiba kulinda na kuimarisha mipaka ya nchi yetu, aidha, JWTZ linatekeleza majukumu yake ya msingi na lina mipaka yake kama yalivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania".