Jumatano , 11th Sep , 2024

Jumuiya ya maridhiano na amani Tanzania imelaani vikali kitendo cha kada wa Chadema kutekwa na kuuawa kikatili lililotokea mwishoni mwa juma lililoisha, huku ikiwataka waliofanya tukio hilo kutotumia uchaguzi kuharibu amani ya nchi yetu.

Sheikh Alhaad Mussa Salum- Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanaznia .

Hayo yamesemwa  Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa Jumuiya ya maridhiano na amani Tanzania, Azim Dewji wakati anaongea na wanahabari leo jijini Dar es Salaam na kuwataka waliofanya vitendo hivyo kutoharibu taswira ya nchi yetu.
"Tukio la utekaji linapotokea na tunajua tunaelekea kwenye uchaguzi hii sio sawa kuchukua uhai wa mtu hakuna mtu mwenye haki ya kuchukua uhai wa mwenzie na kuharibu amani ya nchi yetu, sisi tunalaani vikali kitendo hicho na hatukifumbii macho", alisema Dewji.

Aidha amesema watekaji hao walikuwa wanatoa ishara mbaya kwenye Taifa letu kwani si kawaida utekaji kufanyika mchana.
"Tumezoa kusikia kuwa watu wametekwa usiku lakini hii ya mchana sio kawaida huenda wanatoa ishara fulani au za mwizi ni arobaini kwahiyo hao watekaji siku zao zilikuwa zimefika wakajikuta wamefanya uhalifu mchjana ili wanaswe", alisema Dewji.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanaznia Sheikh Alhaad Mussa Salum, amewataka Watanzania kuwa watulivu kusubiri vyombo vya dola kumaliza uchunguzi ili kujua nani aliyehusiska na vitendo vya utekaji na mauaji ya mwanachama wa CHADEMA.
"Tumeona vitendo vya ukatili vinaendelea kwenye jamii yetu lakini pia tumeona pia kiongozi wa CHADEMA, ametekwa na kuuawa tunakemea vikali na niwatake watanzania tuwe watulivu tusubiri ripoti ya Jeshi la Polisi imalize kazi yake ili waliofanya hilo tukio wachukuliwe hatua", Sheikh Alhaad Mussa Salum- Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanaznia .