Alhamisi , 3rd Dec , 2020

Rais Dkt. John Magufuli, ameahirisha sherehe za maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanzania Bara, ambayo huadhimishwa Desemba 9 kila mwaka, na kuagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo zitumike kununulia vifaa mbalimbali vya Hospitali ya Uhuru iliyopo Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli.

Taarifa hiyo imetolewa leo Desemba 3, 2020, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, na kusema kuwa Rais Dkt. Magufuli, ameagiza kiasi cha shilingi milioni 835,498,700, zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe za maadhimisho ya 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara, zitumike kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya hospitali hiyo.

Novemba 20, 2018, Rais Dkt. Magufuli, aliagiza kiasi cha shilingi milioni 995,182,000.00, zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, tarehe 9 Desemba, zitumike kujenga Hospitali ya Uhuru, ambayo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 92.

Kauli mbiu ya maazimisho ya 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa mwaka huu inasema, "Miaka 59 ya Uhuru na Miaka 58 ya Jamhuri: Tanzania yenye Uchumi Imara Itajengwa na Watanzania Wenyewe, Tufanye Kazi kwa Bidii, Uwajibikaji na Uadilifu.’