Ijumaa , 15th Apr , 2022

Vijana wametakiwa kuchangamkia fursa ya kuomba mikopo ya pesa za Halmashauri zilizotengwa na Serikali kwenye kila Halmashauri ili kusaidia Vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Diwani wa  kata ya Mbezi juu Anna Lukindo akizungumza na Eatv katika kipindi cha Mjadala

Akizungumza na Eatv Diwani wa  kata ya Mbezi juu Anna Lukindo amesema kuwa, vijana wengi hawana muamko wa kujitokeza kuomba mkopo wa pesa za Halmashauri ili waweze kujikwamua kimaisha, na hivyo kuwataka vijana kuungana makundi na kwenda kuomba mikopo hiyo.

“Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imetenga pesa kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili ziwasaidie kujiajiri, lakini vijana wengi hawana muamko wa kuomba pesa hizo hivyo natoa wito kwa vijana kuunda vikundi vya watu 10 wenye wazo moja ili waweze kukopa pesa hizo zisizo na Riba” Anna Lukindo- Diwani kata ya Mbezi juu.

Ameongeza kuwa, kwenye kata yake ya Mbezi juu tayari mpaka sasa vikundi mbalimbali vya vijana wamepatiwa mikopo ya bajaji na kwamba endapo wakimaliza kulipa wanaweza kukopa tena.

“Kuna vijana kwenye kata yangu wamekopeshwa bajaji 3 na wanalipa kila mwaka, na kama wakimaliza mkopo wanaweza kuongezewa tena lakini kama kutakuwa na kikwazo, kuna nafasi ya kukutana na Afisa maendeleo kwa ushauri” Anna Lukindo- Diwani kata ya Mbezi juu.

Sambamba na hayo amesema kuwa, suala la upatikanaji wa maji safi na salama bado ni changamoto kwenye maeneo mengi lakini tayari Serikali imeanza kuchukua hatua za kuhakiksha vifaa vya usambazaji wa maji vinapatikana haraka.

 “Huduma ya maji imetufikia Mbezi ila kuna changamoto ya vifaa vya kusambazia maji lakini habari njema ni kwamba tayari hatua zimeanza kuchukuliwa na Serikali ili kuhakikisha changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama unatatuliwa” Anna Lukindo- Diwani kata ya Mbezi juu.

Kwa upande mwingine amegusia miundombinu ya barabara, na kusema kuwa kwa asilimia 50 ya barabara za mitaa ya Mbezi juu zimejengwa kwa kiwango cha changarawe huku akisema kuwa kuanzia mwezi wa tano mwaka huu ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami utaanza.