Jumamosi , 19th Jul , 2014

Serikali imeliomba shirika la nyumba la taifa NHC kuelekeza nguvu zake kujenga nyumba kwenye halmashauri mpya kabla ya zile za zamani, ili kukabiliana na ukosefu wa makazi kwa watumishi wanaofanya kazi katika halmashauri hizo.

Waziri, TAMISEMI, Hawa Ghasia

Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu, tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia, ameliomba shirika la nyumba la taifa NHC kuelekeza nguvu zake kujenga nyumba kwenye halmashauri mpya kabla ya zile za zamani, ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa makazi kwa watumishi wanaofanya kazi katika halmashauri hizo.

Waziri ghasia amesema hayo akiwa wilayani mvomero, ambapo amepokea mashine Nne za kufyatulia matofali, interlocking block machines, ikiwa ni sehemu ya mashine 28 zilizotolewa na shirika la nyumba, kwa halmashauri  saba za wilaya zilizopo mkoani morogoro, ambapo pamoja na kushukuru kwa msaada huo unaolenga vikundi vya vijana, na kupongeza wilaya ya Mvomero kwa kununua nyumba tisa za NHC pamoja na uchanga wake, ameahidi wizara yake kusimamia agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuhakikisha kila halmashauri zinatenga maeneo kwa NHC ili wajenge nyumba zitakazonunuliwa na halmashauri na wananchi wengine.

Meneja wa shirika la nyumba, NHC mkoa wa Morogoro, Veneranda Seiff, akikabidhi mashine hizo 28, zilizogharimu shilingi milioni 12, amesema shirika hilo limetoa mtaji wa shilingi laki Tano kwa kila halmashauri kama mtaji na kugharimia mafunzo yatakayotolewa na wataalamu kutoka vyuo vya VETA watakaowafundisha vijana matumizi ya mashine hizo.