Jumatatu , 17th Jul , 2023

Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi, amevitaka vyama vya siasa nchini kutoa ushirikiano katika zoezi la usajili linalotegemewa kuanza Julai 20 mwaka huu huku akikiri ofisi yake kupokea maombi ya vyama 18 vinavyotaka usajili.

Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi

Jaji Mutungi akizungumza na wawakilishi wa vyama vya siasa  kabla ya kuanza kwa zoezi la uhakiki amesema zoezi hilo ambalo mwaka jana lilishindwa kufanyika kutokana na majukumu ya kikosi kazi litafanyika mwaka huu likilenga kukagua hoja muhimu ambazo zilianishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kuhusu maombi yaliowasilishwa kuhusu usajili Jaji Mutungi amesema maombi hayo  ya vyama 18 yatafanyiwa kazi lakini kwanza wakianza kuhakiki vyama vilivyopo kabla ya kupitisha kuendelea na mchakato mwengine.

"Katika hili hatutaki kuona chama kinashindwa kutupa ushirikiano kwa kuwa ni zoezi lenye tija kwa vyama hivyo',' amesema Jaji Mutungi

Nao Profesa Ibrahimu Lipumba Mwenyekiti wa chama cha CUF pamoja na Ana Mlingi Macha Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara wamesema zoezi hilo ni muhimu katika kujenga chama lakini pia ikiwa ni takwa la kisheria .