Jumatano , 15th Nov , 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo amewataka wawekezaji wa biashara ya kaboni nchini kuwa wawazi katika biashara hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo

Ametoa maelekezo hayo wakati wa hafla ya makabidhiano ya hundi ya malipo ya sh. bilioni 4.7 kwa wakazi wa wilaya za Kiteto na Mbulu ambazo zimenufaika na mradi huo mkoani Manyara leo Novemba 14, 2023.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Jafo amewaelekeza wawekezaji kuwa na vyeti vinavyoonesha mahali walipouza bidhaa zao ili kuwa wawazi kwa mujibu wa kanuni ya 4 ya Sheria ya Mazingira inayowataka kuwa na uwazi katika biashara zao.

Kwa muktadha huo amewataka kuwa wawazi zaidi na mchanganuo unaoonesha mwanakijiji na mwekezaji wananufaikaje na Biashara ya Kaboni ambayo inachagiza uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti.

Hali kadhalika Waziri Jafo amefafanua kuwa biashara hiyo inafanyika katika masoko mbalimbali ya hisa, hivyo ameelekeza nitoe maelekezo kila mwekezaji kuweka wazi cheti kinachoonesha mahali alifanya biashara yake.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga amesema Kanuni za Biashara ya Kaboni zilizoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais zimesaidia kusimamia biashara hiyo.

Ameongeza kuwa fedha zitokanazo na biashara hiyo ya hewa ya zimewasaidia kuboresha huduma mbalimbali za kijamiii ikiwemo ujenzi wa zahanati, barabara na shule hivyo zimeisaidia jamii ya Wahadzabe kuwapeleka watoto wao shule.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Heri James ameelezea faida zilizopatikana kutokana na Biashara ya Kaboni kuwa ni kuchochea matumizi bora ya ardhi hivyo kupunguza migogoro ya ardhi.