Waziri Wa kilimo Dkt. Charles Tizeba akisisitiza jambo mara baada ya kutembelea banda la Bodi ya Pamba kwenye maonesho ya kilimo na sherehe za Nanenane Kanda ya Ziwa.
Mwanzo, sikukuu hii ya Nane Nane iliitwa ‘Saba Saba’ ambapo ilikuwa ikiadhimishwa kila tarehe 7 ya mwezi Julai. Baadaye ilihamishiwa Agosti, 8 ya kila mwaka baada ya Saba Saba kufahamika zaidi kwa maonyesho ya wafanyabiashara.
Sikukuu ya maonyesho ya wakulima iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1977 ili kuongezea nguvu sera ya Serikali ya wakati huo ya ‘ Siasa ni Kilimo ‘, ambapo wakulima katika wilaya, mkoa na kitaifa walionesha mazao yao halisi ya kilimo, wakaonyesha pembejeo za kisasa za killimo pamoja na kufundishwa namna ya kutumia pembejeo hizo kwa ustawi wa kilimo na taifa.
Jijini Dar es Salaam sikukuu hii ilitengewa eneo maalum katika barabara ya Kilwa ambapo hutumika mpaka leo kwa maonyesho mbalimbali. Kadri miaka ilivyozidi kwenda mbele sera ya ‘Siasa ni Kilimo’ ilibadilika na kuwa ‘ Siasa ya Kilimo’ na wengine wakiitafsiri kama ‘Kilimo cha Siasa’ kwasababu sikukuu hiyo ilionekana kujaa siasa zaidi huku watu wakilenga kuitumia kibiashara zaidi kuliko malengo ya awali.
Ndipo katikati ya miaka ya 1990 serikali iliamua kuihamisha sikukuu hiyo hadi Agosti nane kila mwaka na kuiacha sikukuu ya Saba Saba kuwa ya wafanyabiashara.
Maonyesho ya Nane Nane kitaifa mwaka huu yanafanyika mkoani Simiyu, katika uwanja wa Nyakabindi, yakiwa yamegharimu takribani Sh 600 millioni. Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ni Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.