
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo, Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamis Kigwangalla
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamis Kigwangalla amesema kuwa serikali itaendelea kutumia sheria zilizopo kwa ajili ya kutoa adhabu kwa wanaofanya vitendo vya udhalilishaji kwa watoto pamoja na kutoa elimu kwa jamii lakini siyo kuwahasi wanaume.
Dkt. Kigwangalla amesema hayo bungeni Mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum CCM, Khadija Aboud aliyetaka kujua , pamoja na serikali kuwa sheria nyingi lakini bado watoto wamezidi kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji, na kuitaka serikali ieleze mkakati mbadala wa kukabiliana na tatizo hilo.
"Serikali itaendelea kutoa elimu pamoja na kufuata sheria ya mtoto ya mwaka 2009 na sheria nyingine za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na matukio ya udhalilishaji wa watoto nchini” Amesema Dkt. Kigwangalla.
Ameongeza kuwa serikali haitawahasi wanaume wanaofanya vitendo hivyo kwakuwa jambo hilo halipo kwenye katiba vilevile ni kinyume na haki za binadamu, bali serikali itaendelea kutoa elimu juu ya madhara ya udhalilishaji kwa watoto na kuitaka jamii iwe mstari wa mbele katika kufichua na kukemea vitendo hivyo hususani kutoa ushirikiano wa kutosha inapotokea kesi kama hizo.
“Familia nyingi hazitoi ushirikiano wa kutosha kuhusu kesi za udhalilishaji wa watoto nchini kwa kuhofia kumpoteza ndugu yao kutumikia kifungo jambo linalokwamisha wahusika kupatikana na hatia kwa kukosa ushahidi wa kutosha” Amesema Kigwangalla.
Aidha Naibu Waziri amesema kuwa watoto ambao hufanyiwa vitendo hivyo husaidiwa kupata usaidizi wa kisaikolojia kutoka kwa wataalam waliopo vituo vya afya pamoja na ustawi wa jamii.
Wakati huo huo akikazia majibu hayo waziri mwenye dhamana ya afya nchini Ummy Mwalimu amesema serikali ipo kwenye mchakato wa kuitaka mahakama, kutenga muda maalum wa kusikiliza kesi za watoto ili ziweze kushughulikiwa kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa serikali imeanza majadiliano na mahakama nchini ili iwe na vipindi maalum vya kusikiliza kesi za watoto na wanawake wanaokumbana na ukatili wa ubakaji na ulawiti ili kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.
Amesema awali walikuwa na mpango wa kuanzisha mahakama za kusikiliza kesi za watoto lakini wameona njia mbadala na ya haraka ni kuwasiliana na mahakama ili watenge muda maalumu kwa ajili ya kushughulikia kesi hizo.