Alhamisi , 18th Dec , 2014

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa serikali anayoingoza haina ubaguzi wa kuchagua maeneo ya kupeleka huduma ila inafanya kazi kwa mujibu wa Ilani na Katiba.

Dkt Ali Mohamed Shein

Rais Shein ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua mradi wa umeme kwa wakazi wa kijiji cha Dongoongwe kilichopo wilaya ya kati na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali na wakazi wa jimbo la Uzini kilipo kijiji hicho ambapo amesisitiza kuwa serikali haichaguzi majimbo wakati wa kupeleka huduma na inafanya kazi kwa kuwatumikia wananchi wote na inahakikisha kuwa huduma muhimu zinawafikia wananchi wote kwa mujibu wa sheria.

Mapema mkurugenzi wa shirika la umeme la Zanzibar Bw Hassan Mbarouk amesema shirika hilo limelenga kufukisha huduma hiyo kwa wananchi wote wa Unguja na Pemba huku akisema gharama za uletaji huo wa umeme umegharimu shilingi milioni 100 ambapo SMZ imetoa milioni 85 na mbunge wa jimbo hilo Mhe Mohamed Seif Khatib ametoa milioni 15, nao wakazi wa kijiji hicho wamesema ndoto yao ya kupata umeme imefanikiwa ambapo kijiji hicho hakijawahi kuona umeme katika makazi yao.

Kijiji hicho ni chamwisho katika jimbo hilo kupatiwa huduma ya umeme ambapo hivi sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imekuwa ikihakikisha huduma za umeme na maji zinawafikia wananchi wa vijijini mbali ya ujenzi wa barabara.