Waziri Lukuvi ameyasema hayo katika mahojiano maalum ambapo amesema upatikanaji wa hati ya ardhi ulikuwa unachukua miezi 6 ukapunguzwa hadi miezi 3 lakini sasa hivi ni ndani ya mwezi mmoja mtu akishalipia ada stahiki serikalini.
''Tumesogeza huduma karibu na wananchi kila kanda tumepeleka makamishna wa ardhi pia kila halmashauri karatasi na mafaili yote ya kujaza hati za kumiliki ardhi yapo, hivyo ndani ya mwezi mmoja mwananchi akishalipia afuate hati yake asipoipata aniandikie barua au anipigie simu''-Amesisitiza Waziri Lukuvi.
Akizungumzia utendaji wa Rais Dkt. John Magufuli, kwa siku 100 Waziri Lukuvi amesema Rais amefanya mambo mengi ambayo hapo awali yalishindikana kufanyika kwa kipindi kifupi cha miezi mitatu.
Kwa upande wa ardhi serikali imeweza kubomoa nyumba za waliovamia viwanja vya masikini, tumebomoa nyumba chini ya usimamizi wa baraza la mazingira kwa wanaoishi mabondeni, tumeweza kurejesha shamba la Kapunga kwa wananchi lililokuwa linamilikiwa na mwekezaji kiasi cha hekari 1870 Wilayani Mbarali.
Pia mashamba makubwa ya mkonge 6 Mkoani Tanga yamerejeshwa kwa wananchi kutoka kwa wawekezaji na kutatua migogoro 200 ya mashamba na viwanja.
Aidha Waziri Lukuvi amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa serikali hii kwani kasi yake katika utendaji itaendelea hivyo hivyo na kwa upande wa wizara yake ni kupima ardhi ya Tanzania nzima na mpango huo unaanzia katika wilaya za Kilombero na Ulanga.








