Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akichangia taarifa ya utekelezaji ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira bungeni jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akichangia taarifa ya utekelezaji ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira bungeni jijini Dodoma.
Amesema kuwa kila halmashauri nchini ni lazima iweke utaratibu mzuri wa zoezi la uzoaji wa taka ngumu na si kuziacha zikizagaa ovyo kwenye mitaa hali inatoweza kusababisha magonjwa.
“Nashukuru kuna yale madampo matano yaliyojengwa katika mikoa mbalimbali kupitia mradi lakini baadhi ya halmashauri bado zinasuasua katika ukusanyaji wa taka..utakuta mtu amepewa tenda (zabuni) halafu hilo lori lenyewe analotumia ni takataka, hili haliwezekani lazima tufikie mahali tutumizi majukumu yetu,“ amesema.
Dkt. Jafo ameongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais jukumu lake ni kusimamia sera wakati halmashauri hizo zinapaswa kutekeleza jukumu lao la kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi.
Akiendelea kuchangia hoja hiyo, alielekeza kuwa majengo yote yanayojengwa hasa katika majiji ni lazima yawe na mifumo ya uvunaji wa maji hatua itakayosaidia kupunguza uharibifu wa miundombinu ya majitaka.
Alisema kuwa miundombinu ya majitaka hasa mifereji inapoharibika husababisha uchafu kukwama badala ya kwenda kwenye mabwawa ya majitaka na hivyo kusababisha mafuriko.
Kwa upande mwingine Waziri Dkt. Jafo alisema kuwa mchakati wa uhuishaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 namba 191 upo katika hatua nzuri na unatarajiwa kukamilika mwaka huu.
Alisema kuwa ni kweli sheria hiyo ina mambo mengi yanayotakiwa kuhuishwa na ni lazima iende na wakati sanjari na Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 ili ikidhi haja.
Hivyo, Waziri Dkt. Jafo alifafanua kuwa Sheria ya Mazingira inayohuishwa imegusa mambo mengi ya msingi yakiwemo mchakato wa kulipa nguvu Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwa mamlaka kamili na kukiimarisha Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC).
Awali akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo, Mwenyekiti wake Mhe. Jackson Kiswaga alisema katika kuhakikisha ukakatiji wa miti unapungua au kuisha kabisa Bunge linaishauri Serikali kuweka ruzuku katika gesi ili wananchi wawe na uwezo wa kumudu kutumia nishati hiyo ambayo rafiki kwa mazingira.
Halikadhalika alisema Bunge linaitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha mchakato wa kuhuisha Sheria ya Mazingira namba 191 unakamilika, ambao unatarajiwa kukamilika mwaka 2024.
Aidha, Mhe. Kiswaga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kalenga alitoa ushauri kwa Serikali iweke mwongozo kwa magari yanayobeba taka ngumu kuyafunika ili zisianguke na kuchafua mazingira.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Regina Qwaray aliiomba Serikali isimamie kanuni na miongozo ya mazingira kukabiliana na wale wanachafua mazingira.
Pia, Mbunge huyo aliipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kusimamia vyema katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki na kuhimizi viwanda viendelee na shughuli ya urejelejezaji wa chupa za plastiki hatua itakayosadia zisizage ovyo na kuchafua mazingira.
Alitahadharisha pia kuhusu uchimbaji wa mchanga na kokoto unafanyika kiholela kwenye makazi ya watu yanatokea na kusababisha makorongo ambayo hufanya mmomonyoko wa ardhi unaosababisha mafuriko.