Jumapili , 3rd Jul , 2016

Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga Godwin Gondwe amesema atasimamia vyema miradi ya maji katika wilaya yake ya Handeni ili wananchi wanaopata tabu ya maji waweze kunufaika na upatikanaji maji.

Gondwe ameyasema hayo baada ya kula kiapo cha uaminifu ambacho wameapishwa wakuu wa wilaya mkoa wa Tanga kiapo ambacho wameongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Martin Shigella.

''Nimeweza kupitia miradi ya maji katika wilaya na kufahamu kuna mradi wa uchimbaji wa mabwawa ya maji hivyo nitasimamia zoezi hilo ili wananchi waweze kupata maji'' amesema Gondwe.

Gondwe ambaye pamoja na kazi nyingine amedumu katika tasnia ya habari kwa muda mrefu, ameripoti katika wilaya yake ya Handeni kuanza majukumu ya ukuu wa wilaya cheo ambacho ni mara ya kwanza kukipata ikiwa ni uteuzi wa hivi karibuni wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigella amewataka wakuu wa wilaya kuangalia fursa zilizopo katika maeneo yao na kuwaunganisha wananchi katika kufaidika na fursa hizo hasa kuwaandaa na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Uganda.