Ijumaa , 3rd Mei , 2024

Jeshi la Polisi Mkoa Morogoro, limewakamata watuhumiwa watatu wa mauaji ya Monica Paul (22), mfanyakazi wa kazi za ndani, mkazi wa Lukuyu Bigwa mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama, akionesha vitu vilivyokuwa vimeibiwa

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoa wa MorogoroSACP Alex Mkama amesema watuhumiwa hao walifanya mauaji hayo Aprili 14,2024 maeneo ya Lukuyu Kata ya Bigwa wilaya na Mkoa Morogoro.

Kamanda Mkama aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mbaraka Omary (25) fundi ujenzi, mkazi wa Tubuyu, aliyekutwa na televisheni aina ya Hisence inchi 60, redio sabufa aina ya Boss, spika ndogo za redio hiyo na feni ndogo aina ya Easy Home vilivyoibiwa siku ya tukio.

Alimtaja mtuhumiwa mwingine ni Mussa Mrisho (23) fundi ujenzi, mkazi wa Bigwa ambaye alishirikiana na Mbaraka Omary kutekeleza mauaji hayo pamoja na Rehema Omary (30) mkulima, mkazi wa Mwembesongo, aliyekutwa na simu ndogo ya marehemu aina ya Tecno.