Fahamu matarajio ya wakenya kwa Rais Samia

Jumanne , 4th Mei , 2021

Wakili Msomi nchini Kenya, Prof. George Wajackoyah amesema kitendo cha mabunge mawili kuungana kumpokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajia pia kuhutubia bunge nchini humo  ni heshima kubwa kwake kwani hutokea mara chache.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

Akizungumza kwenye mahojiano na Kipindi cha Supa Breakfast, cha East Africa Radio, Prof. Wajackoyah amesema miaka miwili iliyopita Waziri Mkuu wa Uingereza alikaribishwa nchini Kenya, lakini hakupata nafasi hiyo ya kuhutubia mabunge yote mawili nchini Kenya.

"Rais Samia atahutubia mabunge yote kwa pamoja hiyo ni heshima kubwa kwa Rais wa Tanzania, kwani hata miaka miwili iliyopita Waziri Mkuu wa Uingereza aliwahi kukaribishwa nchini Kenya, lakini hakuhutubia mabunge yote mawili" amesema Prof. Wajackoyah

Akielezea matamanio ya wananchi wa Kenya, Prof. Wajackoyah ameeleza kuwa wamefurahishwa na ujio huo huku wakimuomba Rais Samia kushirikiana na wapinzani wake katika siasa ili kukuza uchumi na amani ya nchi.

"Watu wamefurahi na wanauliza alisema ataweza kuleta uhusiano mwema kati ya nchi jirani, wamesema wangefurahi sana ikiwa mama Samia angeweza kuhusiana na wapinzani wake wa siasa ili waijenge Tanzania iwe nchi ya amani, Na kuna wale vibaraka hawataki mama aongee na majirani zao ingekuwa vizuri akaanza kujadiliana na wapinzani wa siasa kuleta uchumi, uhusiano mwema na ujirani mwema" amesema Prof. Wajackoyah