Mkuu wa Kitengo cha fedha cha Exim Bank Bw. Selemani Ponda (kushoto) akifafanua jambo katika mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam. Kulia kushoto kwake ni Naibu Mkuu wa Fedha Bw. Issa Hamisi.
Fursa hiyo ni kupitia utoaji wa mikopo ya fedha ikiwa ni pamoja na kwenye mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta unaokusudiwa kujengwa kwa ushirikiano baina ya nchi hizo.
Mkuu wa Kitengo cha fedha cha Exim Bank Bw. Selemani Ponda, amesema hayo leo muda mfupi baada ya kutoa taarifa ya fedha ya benki hiyo kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka, huku Naibu wake Bw. Issa Hamisi akisema kuwa benki hiyo imepokelewa vizuri na wananchi wa Uganda, zikiwa zimepita siku 24 tu tangu kuanzishwa kwake.
"Kama benki inayotoa huduma za kifedha baina ya nchi hizi tupo katika nafasi nzuri ya kuwa moja ya taasisi za kifedha inayoweza kutoa mikopo ya kugharamia mradi huo," amesema Bw. Ponda.
Kwa upande wake, Bw. Issa Hamisi amesema "Tumepokelewa vizuri na Waganda na kwa kipindi cha siku ishirini na nne tu tumeweza kuongeza amana na kufikia fedha za Tanzania bilioni tisini," amefafanua Bw. Hamisi na kuongeza kuwa hiyo ni dalili njema kuwa katika robo ya pili ya mwaka hesabu za benki hiyo zitapanda na kuwa moja ya taasisi kubwa nchini humo.
Kuhusu taarifa ya fedha, Bw. Ponda amesema benki imefanikiwa kupata faida ya shilingi bilioni 53 kabla ya makato ya kodi, huku shilingi bilioni 45 zikiwa zimetokana na mauzo ya hisa katika soko la hisa la Dar es Salaam, wakati shilingi bilioni 8.4 zikiwa zimepatikana kupitia shughuli za kawaida za kibenki.