Jumatatu , 17th Feb , 2025

TANROADS imepanga kupanua barabara za kuingia na kutoka katikati ya jiji la Dodoma zenye jumla ya urefu wa kilometa 220 kwa kuzijenga kwa njia nne na sita kwa lengo la kuhakikisha jiji la Dodoma linaondokana na msongamano wa magari na kusaidia kuboresha huduma za usafiri na uchukuzi.

Barabara Dodoma

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Mipango na Miundombinu wa TANROADS, Mhandisi Ephatar Mlavi wakati akielezea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka minne inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Februari 17, 2025.

Mhandisi Mlavi amezitaja barabara hizo kuwa ni Barabara ya Dodoma - Morogoro ambayo itajengwa (km 70), Dodoma - Arusha (km 50), Dodoma - Singida (km 50) na Dodoma - Iringa (km 50).

"Nia ni kuhakikisha barabara hizi zinaungana kwa urahisi na barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma ‘Dodoma Outer ring Roads’ na hivyo kulifanya jiji la Dodoma kuwa la mfano lisilo na msongamano wa magari na hivyo kuvutia shughuli za ukuaji wa uchumi," amesema Mhandisi Mlavi.

Mhandisi Mlavi amefafanua kuwa upanuzi wa barabara hizo utatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na utekelezaji wake utaanza na barabara zinazoingia na kutoka katika jiji la Dodoma kuelekea Chamwino (km 32), barabara ya Dodoma kuelekea Iringa- Mkonze (km 4.5) na barabara ya Dodoma kuelekea Arusha - Zamahero (km 8.5).

Aidha, Mlavi ameeleza kuwa hadi kufikia Februari, 2025 utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya mzunguko (km 112.3) sehemu ya kwanza ya Nala – Veyula – Mtumba - Ihumwa Bandari Kavu (km 52.3) umefika asilimia 91 na sehemu ya Pili ya Ihumwa - Bandari Kavu – Matumbulu - Nala (km 62) umefika asilimia 85.