Dkt. Biteko ametoa agizo hilo tarehe 15 Novemba, 2023 mkoani Mtwara wakati alipokagua miradi ya umeme vijijini na kuwasha umeme katika Kata ya Naliendele, eneo la Pachota A na Kijiji cha Nachenjele.
"TANESCO na REA, tabia ya kununua vifaa vya umeme nje ya nchi hiyo ni zilipendwa, viwanda vipo ndani ya nchi halafu vifaa vinanunuliwa nje, hivi vifaa vyetu mnataka tukauze wapi, kuanzia leo na kuanzia nilivyoingia ndani ya ofisi lazima bidhaa zinazozalishwa hapa zinunuliwe na vifaa visivyopatikana ndani ya nchi ndio viagizwe kutoka nje, tukuze viwanda vyetu, tuvipe thamani na kukuza ajira." Amesema Dkt. Biteko
Aidha, Dkt. Biteko amewataka wakandarasi wa umeme vijijini kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kueleza kuwa Serikali itafanya tathmini ya kila mkandarasi kuona alivyotekeleza miradi na ambao hawafanyi vizuri watasitishiwa mikataba kwani Serikali inalipa wakandarasi hao na itaendelea kuwalipa hivyo hawana sababu za kukwamisha Miradi ya Upelekaji Umeme Vijijini.
"Angalieni mabilioni yaliyomwagwa kwenye Mkoa wa Mtwara, shilingi bilioni 170 zimeletwa hapa kusambaza umeme vijijini ambazo zitafaidisha pia maeneo ya mijini lakini yanafanana na kijijini, lengo letu ni mwezi wa sita mwakani kumaliza kazi ya kupeleka umeme vijijini na kuhamia vitongojini." Amesema Dkt. Biteko
Pamoja na kuwapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kusimamia vyema kazi ya kusambaza umeme, amewataka kutokucheka na wakandarasi hao ili kazi ya kupeleka mahitaji ya umeme kwa wananchi ifanyike kwa ufanisi.
Katika katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaeleza wananchi wa Mtwara juhudi mbalimbali zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwapelekea maendeleo kama vile ujenzi wa miundombinu ya kielimu, afya, barabara na upanuzi wa bandari ya Mtwara .