Jumamosi , 30th Sep , 2023

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko ameendelea na ziara yake ya kikazi katika mikoa mbalimbali nchini ambayo imejumuisha kuwasha umeme katika baadhi ya vijiji vya Bukombe mkoani Geita, Biharamulo, leo amewasha umeme katika kijiji cha Ntanga na Kasharazi wilayani Ngara

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Ntanga wilayani Ngara Mkoa wa Kagera wakati alipofika kuwasha umeme kwenye kijiji hicho.

Akizungumza na wanachi katika kijiji cha Ntanga na Kasharazi, amesema kuwa, Wilaya ya Ngara ina vijiji 75 ambapo mpaka sasa vijiji 43 tayari vina umeme na kwa vijiji ambavyo bado havina umeme, amewaagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa, vijiji hivyo vinapelekewa umeme na baadaye kuanza mpango wa kupeleka umeme kwenye vitongoji.

Amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 49 kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini mkoani Kagera ikiwemo wilaya ya Ngara hivyo amewaahidi wananchi kuwa umeme utafika kwenye maeneo yote.
Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko ameagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na wakandarasi wa umeme kuhakikisha kuwa wanatoa kipaumbele cha matumizi ya vifaa vya umeme vinavyozalishwa ndani ya nchi ikiwemo nguzo, mita na transfoma.

“Nchi hii tulihamasisha ujenzi wa viwanda vya kuzalisha vifaa vya umeme, lakini muda mwingi utaona tunajishughulisha na kununua vifaa nje ya nchi, tunatumia Dola nyingi kuagiza vifaa vya umeme wakati tuna viwanda vipo ndani, natamani mjengee uwezo viwanda vyetu vya ndani ili viweze kuzalisha zaidi na hivyo tukuze uchumi wa watu wetu.”amesema Dkt. Biteko

Amesema kuwa, viwanda hivyo vimejengwa ili viweze kusambaza vifaa kwa TANESCO, REA na wakandarasi wa umeme hivyo si sahihi kwa vifaa hivyo kuagizwa kutoka nje ya nchi.

Akiwa katika Kijiji cha Kasharazi, Dkt.Biteko ametoa kompyuta 10 kwa shule ya sekondari Rusumo B ambayo imeunganishwa na umeme ili kuanzisha darasa la kompyuta katika shule hiyo ambapo pia amewaasa wanafunzi hao kuwa kuwa na nidhamu na juhudi katika masomo.