Jumanne , 23rd Jul , 2019

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dkt. Bashiru Ally amesema wana CCM watakaofanya marumbano ya rejareja yanayoendelea hivi sasa, hawatasita kuwachukulia hatua mara moja na kwamba waige mfano wa kukaa kimya kama afanyavyo kiongozi wao.

Dkt. Bashiru ameyabainisha hayo leo Julai 23, mkoani Dodoma, wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho katika uzinduzi wa vibanda vya biashara, ambapo amesema kazi ya kulinda, chama, ushindi ama kukijenga chama hicho ni ya wana CCM na ni kazi ya kufa na kupona.

''Wapuuzeni hao wapumbavu, hatuogopi kukosolewa sisi, lakini hatuko tayari kudharauliwa, kutukanwa na kubezwa na kuitwa majina ya kejeli kwa watu wasiokuwa na shukrani, hatujafunzwa hivyo, hatujazoea hivyo, nachowaomba wana CCM jifunzeni kwa kiongozi wetu, wakati wote hana muda wa malumbano na amevumilia matusi'' amesema Dkt. Bashiru Ally.

Aidha amewataka wanachama hao wasitumie maneno yaliyopo sasa kama ''Kiki'' kwa kujifanya wao ndio makada kuliko wengine.

''Maana kuna watu hapa watataka kuutumia upuuzi unaoendelea kujifanya wao ndiyo makada kuliko wengine, tunazo taratibu, kanuni na katiba yetu na miiko yetu, ole wake mwana CCM yoyote atakayetaka kutumia fursa ya upumbavu wa wapumbavu wa mwaka kutafuta kiki ya kisiasa ili achaguliwe kwenye Serikali za mitaa'' amesema Dkt Bashiru.