Jumatano , 29th Oct , 2025

Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo Jumatano, Oktoba 29, 2025, amejitokeza kupiga kura katika Kituo cha Kariakoo, Jimbo la Kwahani, Unguja, akitimiza haki yake ya msingi ya kikatiba kama raia wa Zanzibar.

 

Dk. Mwinyi aliwasili kituoni hapo majira ya saa 2:15 asubuhi, na kuungana na wananchi wengine waliokuwa kwenye foleni, hatua iliyopokelewa kwa heshima kubwa na tafsiri ya wazi ya kuzingatia misingi ya usawa, demokrasia na utulivu wa kisiasa.

Wananchi waliomshuhudia wakimpongeza kwa kuonyesha unyenyekevu, uzalendo na heshima kwa taratibu za uchaguzi, licha ya nafasi yake ya juu ya uongozi. Ujio wake uliongeza hamasa kituoni hapo huku ukitafsiriwa kuwa ni ujumbe wa amani, mshikamano na haki kwa kila Mtanzania.

Tukio hili limeendelea kuonyesha dhamira ya viongozi wa kisiasa kuimarisha imani ya umma kwenye mifumo ya uchaguzi huru na wa haki.