Jumatatu , 23rd Dec , 2019

Watanzania waishio nchi za Nje (Diaspora), wapo kwenye mkakati wa kujenga daraja lenye urefu wa Kilomita 30.01, kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar, ambapo wamependekeza daraja la kuelea kwasababu ujenzi wake ni rahisi na gharama zake ni nafuu na garantii yake ni miaka 100.

Muundo wa daraja ambalo limependekezwa kujengwa juu ya Bahari kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar.

Tarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Diaspora Duniani, Norman Jasson, wakati wa kongamano la sita la Diaspora, lililofanyika visiwani Zanzibar, na kusema kuwa kwa sasa wanasubiri baraka kutoka Serikali ya Tanzania ili kuanza upembuzi yakinifu wa kujua gharama za ujenzi wa daraja hilo na kwamba wanafanya hivi ili kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

Jasson amesema kuwa daraja hilo litakuwa na njia tatu, moja ni kupitisha magari yanayotoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar na njia ya pili ni magari yanayotoka Zanzibar kuja Dar es Salaam na njia ya tatu ni kwa ajili ya watembea kwa miguu na waendesha baiskeli. 

Aidha katika majadiliano yao waliweka mapendekezo matatu ya ujenzi wa daraja hilo, ikiwemo, kujenga daraja la kupita ndani ya Bahari, pili daraja la kupita juu na tatu ni daraja linaloelea majini, ambalo ndilo lililopendekezwa.

Kwa mujibu wa Diaspora daraja la ndani ya maji halikuchaguliwa kwasababu, ndani ya maji kati ya Dar es Salaam hadi Zanzibar kuna mkondo wa maji na maporomoko, ambapo pia hawakuweza kuchagua daraja la juu kwasababu, Bahari ya Hindi eneo hilo kuna kina kirefu. 

Akizungumza leo Disemba 23, 2019, Makamu Mwenyekiti wa umoja wa Diaspora Duniani (TDC), Edwin Ndaki, amesema kuwa ni kweli mpango huo upo na kwamba wanahitaji Serikali ya Tanzania iwaunge mkono.

"Tanzania Diaspora wanapenda kuiomba Serikali ituunge mkono ili tuweze kuchangia zaidi utaalamu na fedha, lakini pia tunaishukuru Serikali kwa kukamilisha sera yetu ni matumaini yetu tutazidi kushirikiana ili kufungua fursa zaidi kwa Diaspora kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo na ujuzi walioupata nje" amesema Ndaki.