Jumanne , 21st Mei , 2024

Kutokana na kuwepo wa taarifa za wizi unaotokea katika maduka mengi wilayani Songea huku sababu zikiwa makampuni ya ulinzi ya manispaa hiyo kuajili walinzi wengi wenye umri mkubwa wanaoshindwa kukabiliana na wezi, serikali ya wilayaimetangaza msako wa kugagua makapuni yaliyoajiri wazee.

Wilman Kapenjama Ndile, Mkuu wa Wilaya ya Songea

Akiongea na EATV Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Wilman Kapenjama Ndile amesema sheria ya ulinzi inakataza mtu aliyezidi umri wa miaka 55 kufanya kazi ya ulinzi hivyo serikali ya wilaya itafanya msako kukagua makampuni ambayo yameajili walinzi wenye umri mkubwa huku SSP Kabis Kirangi ambaye Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Songea amesema changamoto nyingine iko kwa wamiliki wa makampuni ya ulinzi kutoa bunduki ambazo hazina risasi na walinzi wengine hawana silaha kabisa.

Kwa upande wao wamiliki wa makumpuni ya ulinzi wa wilaya humo wamesema changamoto kubwa iko kwa wafanyabiashara ambao hawataki kutoa gharama kwa ajili ya ulinzi hali inayosababisha kuwatumia walinzi wenye umri mkubwa huku mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoa wa Ruvuma akisema huu ni wakati wa kushirikiana kati ya jeshi la polisi makampuni ya ulinzi pamoja na wafanyabiashra ili kuiondosha changamoto hiyo.