Jumatatu , 27th Aug , 2018

Imeelezwa kuwa chaguzi ndogo zinazoendelea zimepelekea uvunjifu wa amani baadhi ya sehemu kutokana na namna uchaguzi huo unavyoendeshwa huku lawama nyingi zikielekezwa kwa tume ya taifa ya uchaguzi kwa  kuwa sio tume huru ndio chanzo cha wananchi kukosa imani.

Akizungumza kwenye East Africa BreakFast ya East Africa Radio mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Dkt. Albane Marcus amesema kuwa migogoro mingi ya kisiasa katika nchi za Afrika inasababishwa na kutojitosheleza kwa katiba zinazoongoza nchi za kiafrika.

"Vyama vya upinzani kugomea uchaguzi wa marudio haiwezi kusaidia kutatua changamoto ambazo wamekuwa wakilalamikia katika chaguzi mbalimbali kwa kuwa hawatokuwa wakiwatendea haki wapiga kura wao", amesema Dkt. Albane.

Dkt. Albane ameongeza kuwa upinzani kazi yake ni kuikosoa serikali ili kuisukuma kufanya miradi ya maendeleo na sio uadui na chuki.

Hayo yamejiri ikiwa ni siku chache tangu vyama vya CHADEMA, ACT Wazalendo na NCCR Mageuzi kutangaza kugomea kushiriki uchaguzi wa udiwani katika Kata ya Mwanzage jijini Tanga kwa kile walichoeleza ni kuwepo kwa zuio la mahakama juu ya uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC), uchaguzi wa udiwani na wa mbunge katika kata na majimbo yaliyotangazwa utafanyika Septemba 16, mwaka huu