Ijumaa , 1st Jul , 2022

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. John Jingu, ametoa wito kwa, taasisi mbalimbali za serikali, kiraia na wadau mbalimbali wa maendeleo kuunganisha nguvu  dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. John Jingu

Wito huo umetolewa katika kikao cha dharura cha Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta wa Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) kilichoongozwa na Mwenyekiti wake Dkt, John Jingu Mjini Dodoma.

“Tumefanya tathmini kuhusu hali halisi jinsi ilivyo kuhusu ukatili, changamoto bado zipo na tumekubaliana tuunganishe jitihada, kwa kufanya kazi kama timu katika kupambana dhidi ya ukatili wa wanawake na Watoto,"amesema Dkt. Jingu.

Aidha Dkt. Jingu ameongeza, "Tumekubaliana kuongeza kasi ya utekelezaji katika maazimio mbalimbali ambayo tumekubaliana na jitihada hizi tutaendelea kuzifanyia kazi na tathmini kila wakati ili kutokomeza ukatili dhidi ya watoto,"

Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainabu Chaula, amesema tunapaswa kupaza sauti dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto kuanzia umri usiojitambua mpaka wa kujitambua.

"Janga hili liko kwenye ngazi ya kifamilia, tafiti zinaonesha ukatili mwingi unaofanyika dhidi ya watoto unazimwa katika ngazi ya kifamilia kwa sababu ya kuogopa kuleta migogoro, watoto hawa ambao hawana hatia unawasababishia kupata sonona, na utu uzima usioeleweka," amesema Dkt. Chaula.