Alhamisi , 11th Mei , 2023

Umoja wa Mataifa umesema takribani mtoto mmoja kati ya 10 huzaliwa kabla ya wakati wake duniani kote na karibu mtoto mmoja kati ya 13 kati yao hufariki kutokana na matatizo yanayosababishwa na kuzaliwa kabla ya wakati.

Hayo yameelezwa katika ripoti iliyotolewa Jumatano mjini Gevena na Shirika la Afya Duniani, WHO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF na Muungano wa Mashirika yanayohusika na Afya ya Mama, Mtoto mchanga na Mtoto, PMNCH.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa kati ya mwaka 2010 na 2020, watoto milioni 152 walizaliwa kabla ya wakati. Watoto hao ni wale ambao wanazaliwa kabla ya wiki ya 37 ya ujauzito, wa kawaida wa wiki 40.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, suala la mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati kuendelea kuishi, linategemea mahali alipozaliwa. Kwenye nchi zenye kipato cha juu, tisa kati ya watoto 10 wananusurika, hata ikiwa walizaliwa chini ya wiki ya 28 ya ujauzito. Lakini kwenye nchi zenye kipato cha chini, ndiko kuna visa vya mtoto mmoja tu kati ya 10.