Mwenyekiti wa Chama cha madereva wa Malori Tanzania (CHAMAMATA) Clement Masanja
CHAMA cha madereva wa Malori Tanzania (CHAMAMATA) kimetoa siku 90 kwa halmashauri ya wilaya ya Longido, kuwaboreshea mazingira mazuri madereva wanaopitisha mizigo, mpaka wa Namanga, ikiwemo ujenzi wa
choo, bafu na mahali pa kupumzikia, vinginevyo baada ya siku hizo watasitisha kutoa huduma za usafiri.
Agizo hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania, Clement Masanja, wakati akizungumza katika kikao kilichowakutanisha madereva wa malori , halmashauri, viongozi wa chama hicho na mamlaka
ya mapato Tanzania (TRA) na usalama barabarani, kilichofanyika mpakani Namanga wilayani humo.
Masanja amesema lengo la kukutana ni kuzungumzia kero wanazokumbana
nazo madereva, katika safari zao kupitia mpaka huo, ikiwemo ukosefu wa
choo, bafu na mahali pa kupumzikia, hali inayosababisha madereva hao
kupata adha kubwa.
Amesema madereva kila wanapopita mpakani hapo, wamekuwa wakitozwa ushuru wa shilingi 5,000 na halmashauri hiyo, wakati
wa kwenda na kurudi hutoa hiyo hiyo, ambapo fedha hizo ni kwa ajili
ya maendeleo ya eneo husika, sambamba na kuwaboreshea mazingira madereva hao kwa kujengewa vyoo,bafu na mahali pa kupumzika .
Pia amesema mbali na fedha hiyo pia wanashangaa kutozwa shilingi elfu
moja wanapotaka huduma ya choo na kuoga kwenye baa za eneo hilo, jambo linalowanyima raha.
Masanja amesema kero nyingine ambayo wamekuwa wakikumbana nayo
ni kitendo cha wao kulipa fedha nyingi, barabarani na kuwafanya mwisho
wa siku kujikuta hawana hela ya kutumia kulingana na kiasi kidogo cha
fedha walichopewa na waajiri wao, hivyo kuwaweka katika wakati mgumu
sana .
Amesema kuwa, kufuatia hali hiyo wamekubaliana na halmashauri hiyo
kuandika barua, zitakazoeenda kwa waajiri, kuhusu malipo hayo ya
ushuru wa shilingi 10,000 ili waajiri wawajibike kulipia fedha hizo wenyewe na sio kuwaachia madereva kama ilivyokuwa .
Pia chama hicho kimepiga marufuku ulipishwaji wa fedha hiyo, unaofanywa kati ya mpaka wa Kenya na Tanzania kwa madereva, kwa ajili ya kuwajazia nyaraka mbalimbali za kuendelea na safari ambapo ni jukumu la madereva wenyewe kujaza nyaraka hizo na sio kusaidiwa na mawakala wanaowalaghai na kuwalipisha fedha hizo.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa halmashauri ya Longido, Mweka hazina
wa wilaya hiyo, Issa Mbilu amesema ameyapokea malalamiko yote ya chama hicho na hivyo atayapeleka maagizo hayo, kwa viongozi husika na kuweza kufanyiwa kazi mara moja.