Ijumaa , 15th Dec , 2017

Katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Dkt. Vicent Mashinji amesema Ufisadi sio agenda pekee ambayo chama chake na upinzani wanashughulika nayo.

Mashinji ameyasema hayo kufuatia taarifa ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Siha kwa tiketi ya CHADEMA Godwin Aloyce Mollel kueleza kuwa amejiuzulu uanachama ndani ya CHADEMA pamoja na Ubunge ili kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika kupambana na ufisadi.

“Ameongelea sana kwamba kuunga mkono hoja za Ufisadi, lakini si kweli kwamba agenda za upinzani ni Ufisadi peke yake tulikuwa na agenda mbalimbali mojawapo ikiwa ni jinsi gani taifa letu litapata viongozi”, amesema Mashinji kwenye mahojiano na kituo kimoja cha Televisheni.

Aidha Katibu huyo ameongeza kuwa upinzani unazidi kuimarika katika taifa hili na umeendelea kubeba agenda za wananchi katika kutoa mtazamo mbadala katika kuleta maendeleo.

Siku za hivi karibuni upinzani umeondokewa na wabunge wake kadhaa akiwemo aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kinondoni Maulid Mtulia (CUF) pamoja na Godwin Aloyce Mollel ambaye alikuwa Mbunge wa Siha (CHADEMA). Mtulia tayari ameshajiunga na CCM wakati Godwin naye akiweka wazi nia yake ya kujiunga na CCM.