Jumanne , 19th Dec , 2017

Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Adam Kimbisa kupitia CCM, amewekewa pingamizi kugombea nafasi ya Spika  wa Jumuiya hiyo na muwakilishi kutoka Uganda Freddy Mbidde kwa madai ya kupokezana uongozi.

Uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki ulipangwa kufanyika jana, lakini kutokana na demokrasia ya kila nchi iliyopo katika jumuiya hiyo kupata kiongozi, nchi ambayo imewahi kuongoza itaruhusiwa kurejea tena pindi kila nchi itakapo kamilisha kupata muwakilishi. 

Abdulrahman Kinana ndiye Spika wa  kwanza wa Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki tangu  ianzishwe mwaka 2001, ambapo alihudumu kwa miaka mitano kama katiba inavyotaka, akafuatiwa na Abdirahim Abdi kutoka Kenya kisha akafuatia na Margaret Zziwa wa  Uganda.

Wagombea ambao tayari wamechukua fomu ni pamoja na Leontine Nzeyimana  kutoka Burundi, Adam Kimbisa kutoka Tanzania, Dkt. Martin Ngoga kutoka Rwanda wakati Sudani Kusini haikutoa mgombea.

Katibu Mkuu wa Bunge hilo Kenneth Madete ameamuru uchaguzi huo ufanyike leo Desemba 19 saa nane na nusu mchana ili kupisha majadiliano ya kuweza kupata wagombea nafasi ya Spika wa bunge asiyekuwa na mgogoro.