Jumamosi , 27th Jun , 2015

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuahirishwa kwa tarehe ya kuanza kwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Mikoa ya Dar es salaam na Pwani hadi hapo itakapotangazwa tena.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuahirishwa kwa tarehe ya kuanza kwa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Mikoa ya Dar es salaam na Pwani hadi hapo itakapotangazwa tena.

Taarifa kwa Vyombo vya Habari iliyotolewa na Tume hiyo na kutiwa saini na Mkurugenzi wa Uchaguzi Bwana Julius B. Mallaba leo imesema hatua hiyo imetokana na kuchelewa kuwasili kwa vifaa vya kuandikishia Wapiga Kura (BVR), ambavyo viko katika Mikoa ambayo zoezi la Uboreshaji linaendelea.

Taarifa hiyo imeendelea kufafanua kuwa Tume imelazimika kupeleka vifaa vilivyotarajiwa kutumika katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani , kwenda katika mikoa iliyoonesha kuwa na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hali inayotafsiriwa kuwa ni kuongezeka kwa mwamko miongoni mwa wananchi wanaojitokeza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Awali Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia Teknolojia ya “Biometric Voters Registration” (BVR) kwa Mkoa wa Pwani ulipangwa kuanza tarehe 25/06/2015, Aidha kwa Mkoa wa Dar es salaam Uandikishaji ulitegemewa kuanza tarehe 04/07/2015.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa rai kwa wananchi wa Mikoa ya Pwani na Dar es salaam kuwa watulivu wakati ambapo ikisubiri vifaa vya Uandikishaji kutoka katika Mikoa itakayokuwa imekamilisha zoezi hilo.