Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini LHRC Dkt. Hellen Kijo Bisimba akifafanua jambo.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini LHRC kimesema kikao cha Bunge la 11 mkutano wa 3 kilichoisha tarehe 30.06.2016 kimekuwa na changamoto nyingi sana ambazo zimepeleka watanzania kukosa haki zao za msingi hasa kutokurushwa moja kwa moja kwa vikao hivyo na kuwepo kwa lugha za maudhi ndani ya bunge hilo na kupelekea kukosa maelewano katika utoaji wa maamuzi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini LHRC Dkt. Hellen Kijo-Bisimba alipokua akizungumza na East Africa Radio na kuongeza kuwa ukosefu wa nidhamu kwa baadhi ya wabunge ndio umepelekea kukosekana kwa maelewano ndani ya Bunge hilo na kupoteza dira.
Amesema kati ya changamoto ambazo zimekwenda kinyume na sheria na haki za binadamu ni pamoja na matumizi mabaya ya muda wa kuchangia vitu visivyofaa kwa wananchi,baadhi ya wabunge kukosa imani na Naibu Spika na kupelekea kuwepo kwa hoja binafsi za kumkataa naibu Spika na baadhi ya kanuni za Bunge kutokufuatwa.
Aidha amesema niwajibu kwa viongozi wa Bunge kuongoza Bunge kwa kufuata sheria na kanuni zinavyoelekeza kwa kuondoa masuala ya vyama katika kutoa maamuzi mbalimbali ya nchi.
Kwa upande wa suala la Bajeti ya 2016/2017 Dkt. Kijo-Bisimba ameishauri serikali kuhakikisha bajeti hiyo inapatikana kwa kuwapa watanzania unafuu wa maisha na sio kuwaumiza watanzania wa vipato vya chini ambao hawana uwezo wakuzipata fedha hizo.
Katika adhabu mbalimbali ambazo zimetolewa kwa baadhi ya wabunge waliokiuka taratibu za Bunge amesema zimekuwa zikitolewa kwa matabaka na kukosa usawa wa kisheria.



