Alhamisi , 1st Mei , 2014

Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi taifa, Abdallah Bulembo ameagiza shule zote zinazomilikiwa na jumuiya hiyo nchini Tanzania kukata bima ya moto kwa lengo la kuchukua tahadhari ya majanga ya moto sambamba na kuwa na uhakika wa kupata fidia ya mali.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya chama tawala nchini Tanzania CCM, Alhaji Abdallah Bulembo.

Bw. Bulembo ametoa wito huo mara baada ya kutembelea shule ya sekondari ya Ivumwe ambayo inamilikiwa na jumuiya ya wazazi ya chama cha mapinduzi ikiwa ni siku chache baada ya bweni moja la wavulana katika shule hiyo kuteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa.

Mara baada ya kuungua kwa bweni hilo, hivi sasa wanafunzi wanalazimika kutumia vyumba vya madarasa ya kidato cha tano na sita kwa malazi, jambo ambalo linaweza kuathiri maendeleo ya kitaaluma shuleni hapo kutokana na kwamba wanafunzi hao wapo kwenye maandalizi ya mtihani wao wa taifa.