Jumanne , 23rd Dec , 2014

Boti ya Polisi iliyokuwa katika doria Mashariki mwa mkoa wa Kusini Unguja eneo la Jambiani imegonga, mwamba na kusababisha askari waliokuwemo kutoswa baharini huku mmoja akifariki na mwingine hajulikani aliko.

Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar CP Hamdan Omar Makame

Akizungumza visiwani humo Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi CP Hamdan Omar Makame amesema boti hiyo inayoitwa Ushirikiano ilikuwa katika doria ya kawaida na ndipo ilipokutana na dhoruba hiyo na ilikuwa na askari Sita ambapo mmoja wapo akiwa ni afisa wa KMKM, wanne waliweza kuokolewa na mmoja kufariki.

Askari aliyefariki anafahamika kwa jina la Said Hassan Saleh na hadi sasa kikosi cha polisi cha baharini kinandelea kumtafuta afisa wa polisi ASP Tenga Seleman Pandu ambaye bado hajaonekana na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Akizungumzia silaha zilizokuwa ndani ya boti hiyo ambayo ni miongoni mwa boti zilizotolewa msaada na serikali ya Marekani CP Hamdan Omar Makame amesema silaha zote zimepatikana na ziko salama na pia hali ya boti hiyo iko salama na inatarajiwa kuletwa makao makuu ya kitengo cha baharini ili ichunguzwe.

Wakati mwaka 2014 unakaribia kumalizika ajali hiyo ya baharini iliyoikumba boti ya doria ya polisi inaingia katika miongoni mwa ajali zilizosababaisha vifo katika mwaka 2014 Zanzibar.