Jumatatu , 4th Aug , 2014

Bodi ya mkopo ya Elimu ya Juu nchini Tanzania (HESLB) inashughulikia tatizo la wanafunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo ikiwa na baada ya kulalamikiwa na jumuiya ya wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (TAHLISO).

Msemaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Cosmas Mwaisobwa.

Akizungumza na East Africa Radio leo, Mkurungenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi hiyo, Bw. Cosmas Mwaisobwa amesema wanatambua kuchelewa kwa fedha hizo kwa baadhi ya wanafunzi katika programu tofauti katika vyuo vikuu nchini ambapo jitihada zinafanywa na Bodi hiyo kutatua tatizo hilo kwa ili wanafunzi waweze kuendelea na mafunzo yao kwa vitendo.

Hata hivyo Bw. Mwaisobwa hakutoa muda kamili ambao tatizo hilo litashughulikiwa na wanafunzi hao kupatiwa fedha kwa ajili ya mafunzo kwa njia ya vitendo.

Wakati huo huo, imebainika kuwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 14-16 wa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania wanaanza kutumia madawa mbalimbali ya kulevya hali inayotokana na vijana wengi kuwa katika umri wa kutaka kujua.

Akiongea Leo jijini Dar es Salaam mmoja wa vijana wanaofanya uhamasishaji kwa vijana kuacha matumizi ya dawa hizo Karen Dorah amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, MUHAS, asiliamia 14 ya vijana Jijini Dar es Salaam wanatumia dawa za kulevya huku wengi wao wakitumia zaidi dawa za kunusa.

Kutokana na hali hiyo, vijana hao wameitaka serikali kufanya juhudi mbalimbali za kuwanusuru vijana kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kuweka elimu ya dawa za kulevya katika mitaala ya shule za msingi pamoja na kuweka sheria kali kwa watu wanaobainika kusafirisha dawa za kulevya nchini.