Jumatano , 8th Oct , 2025

"Lengo langu, wananchi wenzangu, ni kwa kila kijana, popote alipo, kuwa na fursa zinazomwezesha kupata kazi kwa urahisi au kuwa mjasiriamali," Biya alisema katika hotuba yake.

Rais wa Cameroon Paul Biya mwenye umri wa miaka 92 amejitokeza jana Jumanne katika mkutano wake wa kwanza wa kampeni kwa ajili ya uchaguzi ujao ambapo mkuu wa nchi mwenye umri mkubwa zaidi duniani anawania muhula wake wa nane.

Akihutubia umati wa wafuasi kwenye uwanja wa michezo katika mji wa Maroua Kaskazini mwa Mbali, Biya ameahidi kuimarisha usalama katika eneo hilo linalokumbwa na mashambulizi ya itikadi kali, kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana na kuboresha miundombinu ya barabara na huduma za kijamii iwapo atachaguliwa tena katika kura siku ya Jumapili.

"Lengo langu, wananchi wenzangu, ni kwa kila kijana, popote alipo, kuwa na fursa zinazomwezesha kupata kazi kwa urahisi au kuwa mjasiriamali," Biya alisema katika hotuba yake akiwa katika matembezi ya kwanza katika kampeni ambazo hakuwepo nchini humo kwa sababu alikuwa nchini Uswizi kwa takribani wiki moja.

Hakuna sababu rasmi ya kukaa nje ya nchi ambayo imetolewa lakini Biya amekuwa akisafiri mara kwa mara hadi Ulaya kwenye makazi yake binafsi na kwa ajili matibabu katika miaka ya hivi karibuni. Haonekani hadharani mara nyingi na wakosoaji wanasema uwezo wake wa kutawala umepunguzwa sana na umri wake.

Wakati wa miongo yake madarakani, taifa hilo la Afrika ya Kati lenye takriban watu milioni 30 limekabiliana na changamoto kutoka kwa vuguvugu mbaya la kujitenga magharibi mwa nchi hiyo hadi ufisadi wa kudumu ambao umedumaza maendeleo licha ya utajiri wa maliasili kama vile mafuta na madini.

Angalau asilimia 43 ya raia wa nchi hiyo wanaishi katika umaskini kwa mujibu wa viwango vya msingi vya maisha kama vile mapato, elimu na afya, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.

Bado, Biya huenda akashinda katika uchaguzi huo, haswa baada ya mpinzani wake mkubwa, Maurice Kamto, kuzuiwa kuwania urais mwezi Agosti huku upinzani bado umegawanyika. Chaguzi nyingi zilizopita za Cameroon zimekabiliwa na maswali, huku mamlaka za uchaguzi mara nyingi zikishutumiwa kufanya kazi kwa kumpendelea Biya. Kikomo cha urais kwa mihula miwili kiliondolewa kupitia kura ya wabunge mnamo 2008.