Alhamisi , 16th Mar , 2023

Binti wa miaka 12 amefariki kwa kubakwa na kuchomwa kisu na watu wasiojulikana huko Pasiansi, Manispaa ya Ilemela, Jijini Mwanza.

Inadaiwa wabakaji hao walimvamia usiku anapoishi na bibi yake na kumbaka kisha kumchoma kisu shingoni kitendo kilichompelekea kupoteza  maisha wakati bibi yake akiwa kwenye shughuli zake za kuuza chakula.

Akielezea tukio hilo Bibi wa muathirika wa tukio hilo, Bi Mwanne Hassan amesema alimkuta mjukuu wake akiwa amelala mlango wazi lakini hata alipomuita hakuitika.

 "Nilipomaliza biashara nakurudi ndipo nilikuta mlango wazi, ilikuwa saa saba usiku nikafika nikasema mbona mlango upo wazi? Nikaingia ndani nakumuita lakini hakuitika, nikamshika nikaona amelegea hasemi kitu nikapiga kelele watu wakaja nikawauliza hamkusikia chochote? tulipompeleka pale Sabatho hospitali wakamuangalia kumbe walikuwa wamemjeruhi wamechoma kisu shingoni na kumbaka"

Kwa upande wa mama mzazi wa marehemu  amesema hakuwahi kulitegemea jambo hilo na kwamba limemuumiza kwani binti huyo anayemtaja kuwa ni mwanae wa kwanza alifanyiwa ukatili mkubwa sana.

Mwenyekiti wa mtaa wa Pasiansi Isaya Limbe amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo tukio hilo limetokea na kuahidi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuwabaini wahusika wa tukio hilo