Jumatano , 22nd Apr , 2015

Siku chache baada ya jeshi la polisi mkoa wa Dodoma kufunga vituo vitatu vilivyokuwa vimehifadhi watoto zaidi ya 115 kinyume na sheria mkuu wa wilaya ya Dodoma Betty Mkwasa amesema atafuatilia taarifa za shule za watoto wote waliokamatwa katika vituo

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Betty Mkwasa.

Bi Mkwasa amesema kuwa endapo itabainika kuwepo kwa mzazi au mlezi aliyehusika na kumuachisha mtoto shule ili kujiunga na vituo hivyo atafikishwa mahakamani.

Mkuu huyo wa Wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Dodoma anasema ameamua kuchukua uamuzi huo baada ya kubaini idadi kubwa ya watoto waliokutwa katika vituo hivyo walipaswa kuwa mashuleni

Bi. Betty amesema amesikitishwa na kutokuwepo kwa umoja baina ya wazazi walimu na wanafunzi hatua inayochangia wanafunzi wengi kuhadaika na makundi ambayo yana mirengo ya kihalifu yanayo kwenda kinyume na maadili ya Watanzania.

Mbali na kubainika kuwepo kwa vituo hivyo hivi karibuni kijana wa kitanzania Rashid Mberesero mwanafunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari Biawana manispaa ya Dodoma alikamatwa kwa kuhusika na tukio la kigaidi katika chuo kikuu cha Garrisa nchini Kenya kitendo kilichoacha maswali na taharuki kwa wakazi wa mji wa Dodoma ambao wamewataka vijana kuzingatia masomo na kuepuka tamaa za kufanikiwa kimaisha.

Kwa upande wake Mwalimu Rehema Mbilo ambapo anabainisha kuporomoka kwa maadili kwa wanafunzi kunakopelekea kujiingiza katika makundi ya kihalifu na utumiaji wa madawa ya kulevya ambayo ni matokeo ya wazazi wengi kutofuatilia nyendo za maisha ya watoto ya kila siku, utandawazi na mabadiliko ya mfumo wa maisha.