Jumanne , 15th Apr , 2014

Sehemu kubwa ya barabara zilizoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbali mbali hapa nchini zimeanza kupitika. Tangu jana asubuhi tayari magari madogo yalianza kupitia katika eneo la Ruvu mkoani Pwani.

Waziri Magufuli akishiriki katika usimamizi wa matengenezo sehemu ya daraja la Kizinga latika barabara ya Kilwa huko Mbagala Kongowe.

Sehemu kubwa ya barabara zilizoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbali mbali hapa nchini zimeanza kupitika. Tangu jana asubuhi tayari magari madogo yalianza kupitia katika eneo la Ruvu mkoani Pwani.

Jijini Dar es Salaam barabara ya Kilwa iliyokuwa imejifunga eneo la Mbagala Kongowe katika daraja la Kizinga imeweza kutengenezwa na watu pamoja na magari yalianza kupita tangu jana usiku.

Kwa takriban siku tatu mfululizo uongozi wa Wizara ya Ujenzi pamoja na Watendaji wa TANROADS wameonekana wakihaha mchana na usiku ili kunusuru mawasiliano katika barabara kadhaa ambazo ziliathiriwa na mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha katika maeneo mengi hapa nchini.

Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tayari amefuta likizo za Mameneja wote wa TANROADS na pia kuahirisha mkutanao wa Baraza la Wafanyakazi wa wakala huo ambao ulikuwa ufanyike mapema wiki hii mkoani Tanga, amewataka watendaji hao kurudi katika vituo vyao vya kazi ili wasimamie matengenezo katika maeneo yaliyoathirika..

Jana usiku Waziri huyo wa Ujenzi aliweza kutembelea maeneo kadhaa yaliyoathirika ikiwa ni pamoja na daraja la Mpiji katika barabara ya Dar es Salaam – Bagamoyo, alifika pia huko Mbagala Kongowe ambako sehemu ya barabara ilikuwa imezolewa katika daraja la Kizinga na pia alifika katika eneo la Mtokoti katika barabara ya Kongowe – Mji Mwema ambapo kuna kalvati limekatika lakini wakati huo huo kukiwa na gari kubwa la mafuta limetumbukia.

Tayari katika eneo la Ruvu matengenezo yalikamilishwa jana asubuhi. Kwa upande wa Dar es Salaam ambako Mhe. Magufuli alionekana kushiriki katika usimamizi hadi usiku magari na watu walianza kupita usiku huo huo wa jana katika barabara ya Kilwa.

Kwa hivi sasa jitihada zimeelekezwa katika sehemu ya Mpiji kwenye barabara ya Dar es Salaam – Bagamoyo na eneo la Mtokozi katika barabara ya Kongowe – Mjimwema. Maeneo yote haya yanatarajiwa kuanza kupitika kuanzia leo jioni.