Bango moja kuondoka na Mkurugenzi/Mkuu wa Wilaya

Jumanne , 6th Apr , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekemea tabia ya viongozi wa ngazi za chini kushindwa kutatua kero za wananchi hadi viongozi wa juu watembelee maeneo yao na kukutana na kero ambazo zingeweza kumalizwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia), kushoto ni moja ya bango lenye kero.

Rais Samia ameeleza hilo leo Aprili 6, 2021 Ikulu jijini Dar es salaam wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateuwa Aprili 4, 2021 ambapo amewataka kwenda kushughulikia kero za watanzania.

“Tumezoea tukienda kwenye ziara tunapokewa na mabango ambayo mengi sio ya kushughulikiwa  na viongozi wa juu, naomba bango litakaloonekana wakati viongozi wakuu wakiwa kwenye ziara yawe ni matatizo ya kitaifa, endapo tukikuta kero ndogondogo basi bango moja Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya umwekwenda,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa “Nataka niseme bango moja Mkurugenzi au Mkuu wa Wilaya mmoja amekwenda, na hii haina maana mkazuie watu wakaandike kero zao, maana najua tunapokuja watu wanakuja na mabango mbio mbio mnakwenda kuyakusanya na kuwanyuka watu ili wasiseme yanayowasibu”.

Mbali na hilo Rais Samia amewataka watendaji wa Wizara ya Ardhi kuhakikisha wanatatua migogoro ya ardhi.

“Upande wa Ardhi, watu wameporwa sana ardhi zao na wanaohusika kwenye uporaji ni watendaji wa taasisi wanahusika kutengenezea wezi nyaraka feki, acheni mara moja naomba hili likafanyiwe kazi,” - amesema Rais Samia Suluhu.