Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon akiongea na simu.
Ban ameeleza shukrani zake kwa Rais Kenyatta na watu wa Kenya, kwa ukarimu wao wa miongo mingi kwa idadi kubwa ya waomba hifadhi na wakimbizi.
Katibu Mkuu amemhakikishia Rais Kenyatta kwamba anatambua jukumu na wajibu mkubwa unaoambatana na kuwapa hifadhi wakimbizi wengi, katika mazingira ya changamoto za kiusalama.
Aidha, Ban ametoa wito kwa Rais Kenyatta aendelee kutumia makubaliano ya pande tatu yaliyosainiwa mnamo Novemba 2013, baina ya serikali ya Kenya, serikali ya Somalia, na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kama msingi wa wakimbizi wa Somalia kurejea makwao kwa hiari yao, kwa usalama na kwa utu.
Katika mazungumzo hayo, Ban ametaja kuwa Naibu Katibu Mkuu, Jan Eliasson na Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi, watafanya ziara nchini Kenya mwishoni mwa mwezi Mei, 2016, ili kujadili kuhusu suala hilo, na kusisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa kuchagiza jamii ya kimataifa kuinga mkono Kenya katika kukabiliana na changamoto za wakimbizi.