Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wananchi wa Ruangwa baada ya kuwasili mjini hapo kwa ziara
Amesema suala la kila Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi ni la lazima na si hiari.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jana alipokuwa anazungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Kitandi, Mtimbo, Likunja, Nkowe na Namahema ambako alifanya mikutano ya hadhara.
“Halmashauri ambayo itashindwa kutenga asilimia 10 kwa maana asilimia tano kwa ajili ya vijana na tano kwa ajili ya akinamama, Mkurugenzi wake atakuwa anatafuta safari,” alisema Waziri Mkuu, Majaliwa.
Mhe. Majaliwa yupo wilayani Ruangwa, Lindi kwa ajili ya ziara ya kikazi inayolenga kukagua shughuli za maendeleo, ambapo amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutimiza wajibu wao na serikali haitamvumilia yeyote atakayeshindwa.
Pia Waziri Mkuu amewataka wananchi hao kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili zitakapofika shilingi milioni 50 za kila kijiji zilizoahidiwa na Rais, Dk. John Magufuli waweze kunufaika.
Amesema fedha hizo ambazo zitatolewa kuanzia mwezi Julai mwaka huu zitagawiwa katika vikundi mbalimbali vilivyosajiliwa na si kwa mtu mmoja mmoja hivyo amewataka watendaji wa kata na vijiji kuwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali imefuta tozo tano kati ya tisa za zao la korosho zilizokuwa kero ya muda mrefu na kufanya wakulima wachukie mfumo wa Stakabadhi ghalani.