Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maonyesho hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini, kwa kushirikiana na chama cha wafanyabiashara wa madini nchini TAMIDA, Peter Pereira, amesema hayo jana na kuongeza kuwa maonyesho ya mwaka huu, wanajipanga ili kuhakikisha lengo la kuvutia washiriki linaleta msukumo wa kibiashara
katika Nyanja ya kimataifa.
Pereira ametaja nchi zilizoalikwa katika maonyesho hayo kuwa ni China, Marekani, Thailand, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Canada, India, Japan na Urusi ambazo zitaleta wafanyabiashara wakubwa na kueleza washiriki wake wamethibitisha kushiriki, ambapo wafanyabiashara nchini watapata fursa ya kukukutana ana kwa ana na wafanyabiashara hao wa nje.
Amesema pia wamewaalika wafanyabiashara toka nchi za Afrika Mashariki, kati na kusini, kushiriki maonyesho hayo na kuzitaja nchi hizo Kenya, Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Uganda na Msumbiji, ambao watapata fursa ya kuonyesha aina ya madini mbalimbali yanayozalishwa kwenye nchi zao.
Naye Mwenyekiti wa TAMIDA nchini Sammy Mollel amesema, ili kuhakikisha maonyesho haya yanakidhi haja ya Kimataifa wamewataka wafanyabiashara wa nchini kuleta madini yenye ubora na viwango vya kimataifa, yanayoweza kuingia masoko ya ushindani.
Mollel amesema washiriki pia watapata fursa ya kubadilishana uzoefu katika kuongeza thamani ya madini yao, ili kuleta manufaa ya Kiuchumi baina ya nchi zitakazoshiriki na kukuza mapato yatokanayo na sekta hiyo katika nchi zao.
Mbali na maonyesho hayo, washiriki watapata fursa ya kuonyesha madini aina ya Tanzanite, Green garnet, Rodlight, Almasi na Green Tomaline.
Amesema katika maonyesho ya mwaka jana Octoba 28-30, 2013 nchi zipatazo 29 zilishiriki ambapo jumla ya washiriki 550 walishiriki na madini yenye thamani ya shilingi bilioni 6.9 yaliuzwa na kuniwezesha serikali kukusanya kiasi cha shilingi Milioni 227.4 kama malipo ya mrahaba.