Alhamisi , 15th Jun , 2023

Sijawa Bakari (30) mkazi wa kijiji cha Nangumbu, Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi, ameuawa kikatili kwa kukatwa Koromeo na watu wanaosadikika kuwa ni raia wenye hasira kali baada ya kumtuhumu kuwa ni mwizi wa mazao ya wakulima mashambani

Inaelezwa kwamba, kijana Sijawa alikuwa na Tabia ya wizi ambapo ni siku chache zimepita tangu atoke jela baada ya kutumikia kifungo kwa wizi wa korosho mashambani, Sijawa amerudi kutoka jela Mwaka huu mwezi wa 5.

Kutokana na zao la ufuta kuongezeka bei hadi shilingi elfu 4 kwa kilo, wezi wanaohujumu mazao ya wakulima shambani wamekithiri jambo ambalo linasababisha kuwepo kwa matukio mengi ya wizi na mauwaji katika msimu huu. Wananchi wanasimulia kwamba, walifahamu mienendo ya kijana huyo na kuamua kumfuata hadi nyumbani kwake ambapo walimkuta na shehena ya ufuta, licha ya yeye kutokuwa na shamba lolote.

Wananchi wanasema kwamba, kijana huyo alikuwa akivamia mashambani na kuiba masuke ya ufuta na baadaye kwenda nayo nyumbani ambapo alikamatwa akiwa anakafua ufuta huo (kutoa ufuta kwenye masuke yake).

Baada ya kukamatwa, wananchi walimuongoza kwenda kwenye ofisi ya kijiji lakini njiani kabla ya kufika inasemekana aliamua kujinasua mikononi mwa watu hao na kukimbia, jambo lililowatia hasira wananchi wenye hasira kali na kuamua kumpiga baada ya kumkamata na hatimaye kumuua kwa kumchinja.

#EATV baada ya kuzungumza na vijana ambao ndio tabaka linalotuhumiwa kuhusika na wizi kwa asilimia kubwa lakini pia wepesi kutoa adhabu kali kwa wenzao, wamesema ni ngumu kuepusha kifo kwa mwizi kwani maisha ya sasa ni magumu mno na hakuna yeyote anayeweza kumfumbia macho mtu anayemrudisha nyuma.

 
Aidha, wameitaka mamlaka inayosimamia haki na sheria (Mahakama) Kutoa adhabu kali kwa wezi ili kuwadhorotesha na kuwajengea majuto makubwa warudipo majumbani hivyo kuacha tabia hiyo mara moja.

Jeshi la Polisi mkoani Lindi, limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaasa vijana kufanya kazi halali ili wajipatie kipato huku likiendelea na msako wa kuwapata wale wote waliochukua sheria mkononi na kusababisha kifo cha kijana huo.