Ijumaa , 30th Jun , 2023

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Idedelomkazi, wilayani Mufindi mkoani Iringa Witness Nguvalwa na mtoto wake mwenye umri wa miezi sita wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma baada ya kujeruhiwa kwa kumwagiwa kemikali inayodhaniwa kuwa ni tindikali.

Mwanamke aliyemwagiwa tindikali akiwa kwenye kitanda cha hospitali

Akizungumza kwa tabu akiwa hospitalini hapo Witness amesema mkasa huo ulimkuta aliposhuka kituo cha Maghorofani akitokea Mafinga mkoani Iringa alipokuwa akisubiri usafiri wa kumpeleka atakofikia ili apeleka wito wa Mahakama ya Mwanzo ya Mafinga kwa aliyekuwa mumewe ambaye walitenganishwa na Mahakama hiyo.

Amesema akiwa katika kituo hicho, alipita mwanaume mmoja ambaye hakumfahamu akiwa ameshika kichupa mkononi kilichokuwa na kimiminika na mara baada ya kumsalimia alimmwagia usoni.

Amesema madereva bajaji na bodaboda walimsaidia na kumfikisha kituo cha polisi, ambapo alipewa PF3 na kisha walimpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako amelazwa.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk.Baraka Mponda amesemaa walimpokea mama huyo na mtoto wake wa miezi 6 juzi jioni wakiwa wamejeruhiwa usoni kwa kumwagiwa kemikali.

Dk.Mponda amesema majeruhi hao walifika wakiwa na maumivu makali na mama ameathirika maeneo ya usoni,begani na shingoni na mtoto ameathirika zaidi usoni.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Martin Otieno, amesema wanamshikilia dereva wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Lusajo Makiwelu, kwa tuhuma za kuwamwagia kemikali watu wawili akiwemo mtalaka wake Witness Nguvalwa na mtoto wake mwenye umri wa miezi sita ikiwa ni sehemu ya upelelezi wao unaoendelea.