Alhamisi , 19th Dec , 2019

Chama cha ACT Wazalendo kimeahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa viongozi wa CHADEMA, waliochaguliwa katika awamu mpya ya uongozi ndani ya chama hicho, ukiongozwa na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe.

Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe.

Hayo yamebainishwa leo Disemba 19, 2019, kufuatia taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, wakati wakitoa pongeza kwa Freeman Mbowe, aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti, Tundu Lissu ambaye kawa Makamu Mwenyekiti Bara na Said Issa Mohammed, ambaye amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar.

"Kwenye salamu zake maalum za pongezi Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe, amempongeza Ndugu Freeman Mbowe kwa kuchaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Zitto amewapongeza pia wana CHADEMA kwa kufanikisha Mkutano Mkuu wa Chama chao na kuchagua viongozi wao kwa miaka mitano ijayo" imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa Zitto Kabwe amewahakikishia viongozi waliochaguliwa, utayari wa chama hicho kuendelea kushirikiana na CHADEMA na vyama vingine vya upinzani, katika kuihami Demokrasia ya Nchi, inayotishiwa kuangamizwa na Serikali ya Awamu ya Tano.