Alhamisi , 27th Jun , 2019

Katika hali isiyokuwa ya kawaida akaunti ya Twitter ya Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe, imeeleza msimamo wa Mbunge huyo wa Kigoma Mjini ni kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Kupitia akaunti hiyo ya Twitter imeandika anajua watu watampatia majina mbalimbali kwa uamuzi wake kumuunga mkono Rais Magufuli kama ambavyo imekuwa kwa Mbunge wa Mtama Nape Nnauye.

"Ni kweli tumekuwa tukiikosoa Serikali kwa muda mrefu lakini lazima nikiri kuwa kuna mabadiliko makubwa sana yamefanywa na Serikali hii ya JPM. Japokuwa najua kuna baadhi ya viongozi aliowateua wanamuangusha kiuhalisia Magufuli amefanya mengi." imeandika ukurasa wa Zito Kabwe.

Kupitia ukurasa wa mke wa Zitto Kabwe wa Binti Mwana umeandika kuwa "akaunti ya barua pepe na za mitandao ya jamii za Zitto Kabwe zimedukuliwa, tangu polisi walipochukua simu yake na laptop yake, Zitto amekua hana uwezo wa kutumia akaunti zake za mitandao ya jamii wala barua pepe"

Lakini kupitia ukurasa rasmi wa Chama cha ACT - Wazalendo kimebainisha akaunti ya kiongozi huyo imedukuliwa na watu, na mara ya mwisho simu na laptop ya kiongozi huyo  vilikamatwa na Jeshi la Polisi Visiwani Zanzibar.

Akiwa Bungeni Zitto Kabwe ameeleza kuwasilisha malalamiko yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola kuhusiana na hicho kilichotokea ambapo ameeleza kuwa.

"Nimeshatoa taarifa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola, kwamba juzi msaidizi wangu alitekwa na watu wasiojulikana, najua lengo sio yeye na sasa mitandao yangu ya kijamii kuna jumbe zinatolewa ambazo sio zangu, niwaombe waliomteka wamuachie waje waniteke mimi" amesema Zitto Kabwe

Www.eatv.tv imemtafuta Katibu wa Sera na Mambo ya Nje ya ACT - Wazalendo Idrisa Kweweta kuhusiana na suala hilo ambapo amebainisha chama hicho kuanza uchunguzi wa kumtambua mdukuzi wa taarifa za ukurasa huo rasmi wa Zitto Kabwe.

Sikiliza hapo chini.