
Eneo la Msamvu, Morogoro ilipotokea ajali ya Lori la Mafuta, Agosti 10, 2019.
Miongoni mwa tukio kubwa ni lile la ajali ya Lori la mafuta lililopinduka na kulipuka, baada ya watu kulikimbilia kwa nia ya kuiba mafuta, maeneo ya Msamvu mkoani Morogoro. Tukio hilo lilitokea siku ya Agosti 10, mwaka huu, ambapo zaidi ya watu 60 walithibitishwa kufariki siku ile ile huku wengine zaidi ya 70 wakijeruhiwa vibaya.
Katika tukio hilo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliunda Tume maalumu yakuchunguza ajali hiyo na kwamba hata yeye alikuwa yuko tayari kuwajibishwa, endapo angebainika kufanya uzembe wa aina yoyote ile.
Kwa upande wake Rais Magufuli alituma salamu za pole na rambirambi kwa majeruhi wote wa ajali na Taifa kwa ujumla na kuwataka Watanzania waache tabia ya kuwahukumu, wale waliofariki na wale waliopata majeraha katika ajali hiyo kwani si wote waliokumbwa katika mkasa huo walienda kwa nia ya kuiba.