
Mabaki ya mateka 12 kati ya 28 wa Israel waliokuwa wanashikiliwa huko Gaza wamerejeshwa kwa Israel na Hamas huku ikikiri kuwa inakabiliwa na changamoto kurejesha miili yote na kuishutumu Israel kwa kuendelea kufanya ukiukaji wa kusitisha mapigano.
Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Al Jazeera, Jeshi la Israel limekiuka mara 47 makubaliano ya kusitisha mapigano tangu yalipoanza kutekelezwa mapema mwezi huu wa Oktoba, na kuua watu 38 na kujeruhi 143, kwa mujibu wa maafisa wa Palestina.
Israel inasema kivuko cha mpaka cha Rafah kati ya Gaza na Misri kitasalia kimefungwa mpaka taarifa zaidi itakapotolea huku Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akiishutumu Hamas kwa kutofanya vya kutosha kuopoa miili ya mateka.
Hatua hiyo imekuja katika wakati ambao Kundi hilo likirejesha miili ya mateka wawili zaidi, hii leo, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imetangaza.
Ofisi ya Waziri Mkuu Netanyahu imesema familia za mateka wa Israel ziliarifiwa kuhusu kurejeshwa kwa mabaki hayo,kabla ya miili hiyo miwili kuhamishiwa katika Kituo cha Kitaifa cha Tiba ya Uchunguzi wa Kitaifa cha Israeli kwa utambuzi. "Juhudi za kuwarudisha mateka wetu zinaendelea na hazitakoma hadi mateka wa mwisho arejeshwe," ofisi ya waziri mkuu iliongeza.
Jeshi la Israel liliripoti baadaye kwamba moja ya miili hiyo ilithibitishwa kuwa ya Ronen Tomi Engel. Mzee huyo mwenye umri wa miaka 54 aliuawa wakati wa shambulio la Hamas kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023, na mwili wake ukapelekwa Gaza.
Kufikia sasa Hamas imerudisha mabaki ya miili 12 kati ya 28 ya mateka waliokuwa wakishikiliwa huko Gaza, likiwa ni hitaji kuu la Israel katika mkataba wa wiki moja wa kusitisha mapigano ili kumaliza vita vya miaka miwili.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Hamas ilikuwa iwarudishe mateka wote wa Israel walio hai na waliokufa ndani ya saa 72 baada ya kusainiwa kwake. Kwa kubadilishana, Israel ilipaswa kuachilia miili 360 ya Wapalestina walioaga dunia na baadhi ya wafungwa 2,000 wa Kipalestina.